Wasiojulikana Wamuua Mjumbe – Video

11 0Wasiojulikana Wamuua Mjumbe – Video


MWANZA: Wakati mchakato wa kupitisha majina ya wagombea ubunge kupitia CCM ukizidi kushika kasi, ‘watu wasiojulikana’ wanadaiwa kumteka na kumuua Mwenyekiti wa Tawi la CCM Itilabusiga- Buchosa mkoani Mwanza, IJUMAA linaripoti.

Mwenyekiti huyo aliyefahamika kwa jina la Anthony Gwalagwele, ambaye pia alikuwa mmoja wa wajumbe wa CCM Kata ya Bupandwa katika jimbo la Buchosa, anadaiwa kuuawa na watu hao wakati akivua samaki katika ziwa Victoria.

TUKIO LILIVYOKUWA
Akizungumza na IJUMAA, Mtendaji wa kijiji cha Itilabusiga, Bonivencha Kanyanza alisema tukio hilo lilitokea Agosti 3 mwaka huu, muda wa saa12:30 jioni.

Alisema Mwenyekiti huyo ambaye sasa ni marehemu, katika mtumbwi wake alikuwa ameambatana na wavuvi wenzake wawili waliofahamika kwa majina ya Frank Mang’oha (25) na Ndingi Kaliba (50).

“Wakiwa katikati ya ziwa na wavuvi wenzake, ghafla walivamiwa na watu hao ambao walikuwa na silaha za jadi kama vile; mikuki, mapanga, rungu na fi mbo za chuma, na kuwaamrisha kuwapatia zana zao za uvuvi.

“Licha ya kupatiwa zana hizo ikiwamo mitego ya kunasia samaki, watu hao waliwataka pia kuwapatia simu, jambo ambalo walilitekeleza, lakini ghafla mmoja wa wavamizi hao, alimpiga Mwenyekiti kwa kitu kizito kichwa, kisha akamrukia na kumkaba koo na kumtosa ziwani.

“Wakati purukushani hizo zikiendelea, wale wavuvi wenzake mwenyekiti walikuwa tayari wamewekwa chini ya ulinzi, ndipo mwenyekiti kila alipokuwa akitaka kujiokoa, akawa anapigwa rungu kichwani na kurejea majini. Walimpiga mara tatu kila anapoibuka na baada ya muda hakuibuka tena.

“Ndipo wavamizi hao walipochukua mtumbwi na mitego waliyokuwa wakitumia mwenyekiti na wenziye kuvua, wakatoweka kusikojulikana na kuwaacha wale wavuvi wawili wakielea juu ya maji na kutafuta namna ya kujiokoa,” alisema.

Mtendaji huyo aliendelea kueleza kuwa, kwa mujibu wa maelezo ya Frank Mang’oha na Ndingi Kaliba, wavuvi waliokuwa na mwenyekiti huyo, walipata msaada kutoka kwa mvuvi mwenzao aliyejitokeza na kurejea nchi kavu, kisha wakaenda kuripoti tukio hilo ofi sini kwake. Aidha, Mtendaji huyo aliongeza kuwa matukio hayo hayajawahi kutokea katika kijiji hicho.

“Lakini awali nilisikia taarifa za watu hao pia kuvamia kijiji jirani cha Luhama, hivyo tunaomba jeshi la polisi na vyombo vya dola, kufuatilia matukio haya,” alisema.

MTOTO WA MAREHEMU AFUNGUKA
Mtoto wa marehemu, Anthony Gwalagwele, Paschal Anthony alilieleza IJUMAA kuwa, tukio hilo limewashangaza hasa ikizingatiwa watu hao wasiojulikana, walimvamia baba yake peke yake, na baada ya kuhakikisha amefariki, ndipo walipotokomea.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo, kwa kushirikiana na Mtendaji wa kijiji hicho, waliripoti tukio hilo katika kituo cha Polisi, Kahunda kilichopo katika kata hiyo ya Bupandwa.

“Tumeutafuta mwili tangu siku tukio lilipotokea hadi leo, (juzi), ndipo tumefanikiwa kuupata, tunasubiri taratibu za polisi ili tumuhifadhi baba yetu.

“Tunawashukuru wanakijiji wenzetu, wametusaidia mafuta, mashine na wazamiaji wengine ambao wamefanikiwa kuuopoa mwili wa mzee wetu,” alisema.

Aidha, Mkuu wa Kituo hicho cha polisi Kahunda, Mukama Chibunu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kufafanua kuwa uchunguzi wake unaendelea.

“Muda huu (juzi mchana) ndiyo mwili wa marehemu umepatikana, umepelekwa kufanyiwa postmortem (uchunguzi), ndipo taratibu za mazishi ziendelee.
“Siwezi kukufafanulia zaidi, labda uje ofi sini baadaye, maana sasa mwili unachunguzwa kwanza,” alisema.

CCM WAMLILIA
Akizungumza na IJUMAA, Katibu Mwenezi wa CCM katika tawi hilo la Itilabusiga, Alfred Felician, alisema tukio hilo ni pigo kubwa kwa chama, familia na wananchi kwa ujumla kwa kuwa marehemu alikuwa mmoja wa viongozi shupavu waliokuwa mstari wa mbele kutetea wananchi na chama.

“Alikuwa kiongozi mahiri, kwa sababu alishiriki mchakato wa kura za maoni kwa mbunge wa Buchosa, kutokana na nafasi yake kama mwenyekiti wa tawi, lakini sasa ametuacha na hasa ikizingatiwa alikuwa kiongozi wangu. Kwa kweli ni pigo kubwa sana,” alisema.

 Toa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *