Wauza nyama vibudu watikisa

WAKAZI wa Kijiji cha Ikumbi, Kata ya Bonde la Songwe katika Halmashauri Mji Mdogo wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya Vijijini Mkoani Mbeya, wana hofu kubwa ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kama ya; kuhara, matumbo na kipindupindu kutokana na kutikisa kwa uuzwaji wa nyama vibudu zisizopimwa.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba, baadhi ya wauzaji wa nyama za ng’ombe na kuku, huuza waliokufa (vibudu) ambao hawajapimwa na madaktari wa wanyama. Uchunguzi umebaini kuwa, nyama hizo za ng’ombe na kuku, huuziwa wafanyabiashara ambao hupika supu au kuchoma na kuwauzia wananchi bila kujali hatari inayoweza kutokea.

Afisa wa afya wa kata hiyo, Christina Mesyuuh alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusiana na jambo hilo la kukithiri kwa uuzwaji wa vitoweo vilivyokufa na kama analijua, alikiri kuwepo kwa wafanyabiashara wanaouza nyama hizo. “Jambo hili limejirudia tena mara ya pili, limewahi kutokea mwaka 2007/2008 kwa wananchi wachache kuuza nyama iliyotokana na wanyama waliokufa na yalitokea madhara kiasi,” alisema Mesyuuh.

Aliongeza kuwa mfanyabiashara mmoja mwenye kiwanda cha kuku, walimwandikia barua toka ofisi yao ya afya, kwani walaji waliwahi kuharisha.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Kata ya Bonde la Songwe ambacho ni cha binafsi, Samweli Mwanga alikiri kutokea kwa wagonjwa wanne waliopatikana na kuugua matumbo kutokana na ulaji wa nyama hizo vibudu. “Kati ya wagonjwa wanne, wawili wameruhusiwa na wawili bado wamelazwa wakiendelea na matibabu,” alisema Mganga Mwanga.
Toa comment