Yanga Yataja Upya Siku Atakayotua Yacouba

MJUMBE wa Kamati ya Usajili Yanga na Mkurugenzi Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaambia mshambuliaji wao kipenzi raia wa Burkina Faso, Yacouba Sogne atatua nchini Agosti 31, mwaka huu.

 

Kauli hiyo aliitoa ikiwa ni siku moja imepita tangu mashabiki wa timu hiyo juzi wajazane kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JINA) jijini Dar kumpokea mshambuliaji huyo ambaye baadaye ilishindikana kuwasili.

 

Yacouba ni kati ya washambuliaji wa timu hiyo waliosajiliwa akitokea Asante Kotoko ya Ghana mara baada ya mkataba wake kumalizika na kujiunga na timu hiyo, kama mchezaji huru.

 

Kwa mujibu wa Hersi, ndege yake ilizuliwa kutua nchini hivyo amekatiwa tiketi nyingine na atatoka kwao Burkina Faso Agosti 31, mwaka huu kabla ya siku inayofuatia kutua nchini.

 

Hersi alisema kuwa mshambuliaji huyo mara baada ya kutua nchini, haraka ataungana na kambi ya pamoja kwa ajili ya kuanza mazoezi ya pamoja kujiandaa na msimu mpya wa ligi.

 

“Jana (juzi) hakukuwa na mawasiliano mazuri kati ya mashabiki na uongozi, kwani ndege aliyotakiwa kuja nayo Yacouba ilizuiliwa kutua nchini kutokana na sababu zao.

 

“Hivyo atajiunga na timu Agosti 31 na hatakuwepo kwenye kilele cha Tamasha la Wiki ya Mwananchi litakalofanyika keshokutwa (kesho) kwenye Uwanja wa Mkuu,” alisema Hersi.

 

Katika hatua nyingine Hersi alifungukia mipango ya kuwarejesha kikosi mabeki wakongwe Juma Abdul na Kelvin Yondani kwa kusema kuwa: “Mpaka sasa hakuna nafasi ya Yondani na Abdul kurejea tena Yanga labda kutokee dharura. Usajili wa ndani tayari tumefunga.”

STORI: Wilbert Molandi,Dar es SalaamToa comment