Yondani Kurejeshwa Yanga SC

IMEFAHAMIKA kuwa upo uwezekano mkubwa wa beki mkongwe Kelvin Yondani ‘Vidic’ kurejeshwa kikosini baada ya kuanza mazungumzo upya na uongozi wa Yanga.

 

Beki huyo hivi karibuni alitangazwa kuachwa kwenye sehemu ya kikosi cha msimu ujao akiwa pamoja na nahodha msaidizi Juma Abdul ambao mikataba yao ilimalizika msimu uliopita.

 

Yanga walifikia maamuzi ya kuwaacha nyota hao baada ya kugomea ofa walizopewa awali na hivyo kuruhusiwa wakatafute changamoto sehemu nyingine.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kama mazungumzo yakienda vizuri kati ya uongozi wa Yanga na beki huyo, basi huenda akasaini mkataba kabla ya usajili kufungwa Agosti Mosi, mwaka huu.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa Yanga wanamrejesha kikosini Yondani baada ya kuomba msamaha na kuahidi kuwa sawa kinidhamu mara atakaporejea kikosini.

 

“Upo uwezekano mkubwa wa Yondani kurejeshwa tena kikosini baada ya kufanya kikao na baadhi ya viongozi wa Yanga na kukubali kubadilika katika utovu wa nidhamu ambao mara kwa mara amekuwa akifanya.

 

“Hivyo, yeye mwenyewe amekiri makosa hayo ya kinidhamu na kuahidi kubadilika katika msimu ujao na ndani ya siku chache atasaini mkataba mwingine Yanga,” kilisema chanzo chetu.

 

Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela kulizungumzia hilo alisema: “Bado tunaendelea na zoezi la usajili, hatujafunga rasmi kwani tuna nafasi za kusajili, hivyo kama lipo hilo basi tutaliweka wazi.”

 

Kwa upande wa Yondani, simu yake ilikuwa haipatikani.

WILBERT MOLANDI, Dar es SalaamToa comment